Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule, jana tarehe 15 Septemba 2025 ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ili kuimarisha na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni mradi wa maji wa Miji 28 unaojengwa kwa Tsh. Bilioni 17. Mradi huo ambao una ujazo wa lita 500,000 una lengo la kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama katika Mji wa Chamwino, ambapo utanufaisha kata 4, vijiji 7, vitongoji 48 na jumla ya wananchi 59,000.
Mradi huo unaotarajiwa kukamilika Mwezi Disemba mwaka huu, utaongeza upatikanaji wa maji safi na salama katika eneo la huduma la DUWASA kutoka 91% ya sasa hadi 100%. Aidha, unatarajiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Mji wa Chamwino.
Mradi mwingine uliotembelewa ni ujenzi wa kituo cha afya msanga ambao kwa awamu ya kwanza unahusisha ujenzi wa jengo la mama na mtoto, kichomea taka, vyoo vya wagonjwa na kuanzisha msingi wa jengo la upasuaji. Mradi huo ambao umeanza kutekelezwa mwaka huu 2025 baada ya Halmshauri ya Wilaya ya Chamwino kupokea Tsh. Milioni 250 kutoka serikali kuu, unatarijiwa kunufaisha wananchi 7,650 pale utakapokamilika.
Kadhalika, Mhe. Senyamule ametembelea ujenzi wa daraja la Nzali linalojengwa katika kata ya Chilonwa. Daraja hilo lina kina cha Mita 6.43, urefu wa Mita 60, na upana wa mita 11.4, pamoja na barabara za kuingilia zenye urefu wa kilomita 1.5 ambazo zitajengwa kwa kiwango cha changarawe. Daraja hilo ambalo ujenzi wake umefikia 65% linajengwa kwa Tsh. Bilioni 14.515 na linatarajiwa kukamilika Mwishoni mwa Oktoba mwaka huu 2025.
Vilevile, Mhe. Senyamule ametembelea Shule ya Msingi Chalinze ambapo amekagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu matatu ya vyoo ambayo yamejengwa shuleni hapo.
Hata hivyo, amehimiza wakandarasi wa miradi ambayo ujenzi wake unaendelea kuhakikisha kuwa wanakamilisha miradi hiyo kwa wakati ili ihudumie wananchi, huku akiwataka kuzingatia ubora.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.