Mkuu wa wilaya ya chamwino, Mhe. Janeth Mayanja amekabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Tsh. 132,850,200 kwa vikundi 25 vya wajasiriamali wanawake na vijana ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Mhe. Mayanja amevitaka vikundi vilivyopewa mikopo viitumie kwa tija ili kujiletea maendeleo ya pamoja na ya mtu mmoja mmoja kama inavyokusudiwa na mwisho viweze kufanya marejesho ili vikundi vingine navyo vikopeshwe.
“Hizi fedha siyo zawadi, ni mkopo isiyo na riba ili urejeshaji wake uweze kuwa rahisi. Nawaomba mkazitumie vizuri mpate faida, muweze kujikwamua, ikiwezakana sasa vikundi vianze kupata mitaji baada ya kufanya shughuli za uzalishaji.” Alisema Mh. Mayanja.
Hali kadhalika amewaasa wanachama wa vikundi vilivyopewa mikopo kuwa mabalozi wa mikopo hiyo ili watu wengine nao wahamasike kuunda vikundi na kubuni miradi itakayowawezesha kupewa mikopo.
“Muwaambie wananchi wengine utaratibu mliofuata ili nao waweze kujiunga kwenye vikundi, waweze kutimiza vigezo kama mlivyotimiza nyinyi kwasababu mikopo hii bado ipo na itaendelea kutolewa”.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Dkt. Eusebi Kessy, amevipongeza vikundi hivyo kwa kukizi vigezo vya kupewa mikopo na amevisisitiza kuitumia ilivyokusudiwa.
Vikundi vilivyokabidhiwa mikopo vinajishughulisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji ikiwa ni pamoja na kilimo cha mazao ya chakula, mbogamboga, zabibu, usafirishaji na duka la vifaa vya kuandika (stationery).
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.