Mkuu wa wilaya ya Chamwino, Mhe. Janeth Mayanja amekabidhi vifaa tiba mbalimbali vyenye thamani ya Tsh. 12,194,000 kwa zahanati tano za Mganga, Makoja, Mnase, Itiso, Ikoa. Vifaa tiba hivyo vimetolewa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Improving Tanzania Foundation (ITF) ni pamoja na Mzani wa kupimia watu wazima, seti ya vifaa vya kujifungulia, mashine ya kunyonya uchafu ( sunction mashine) kitanda, kiti cha magurudumu na Mashine ya kupimia presha.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa tiba hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino amemshukuru Mkurugenzi wa ITF Bw. Henrish Madambo kwa kuona haja ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha huduma za afya nchini na amemhakikishia kuwa ofisi yake itahakikisha kuwa vifaa hivyo vitatumika ilivyokusudiwa.
“Niseme tu kwamba vifaa hivi tutavitumia kwa matumizi yaliyokusudiwa kwani kama vifaa vikiwepo lakini huduma zinazotolewa zikawa hafifu, thamanai ya vifaa hivyo haiwezi kuonekana.’
Aidha Mhe. Mayanja amewataka waganga wafawidhi wa zahanati zilizopewa vifaa hivyo kuendelea kuwahudumia wananchi kwa uadilifu, upendo na uzalendo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha matumizi sahihi ya vifaa vilivyokabidhiwa ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Naye mkurugenzi wa ITF amemshukuru mkuu wa wilaya ya Chamwino kwa mapokezi mazuri aliyopewa katika wilaya ya Chamwino na ameahidi kuendeleza ushirikiano katika kutekeleza miradi mingine ya maendeleo ili kuboresha maisha ya wananchi.
Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Dkt. Euseby Kessy ambaye pia ametoa shukrani kwa wadau hao kwa kutoa vitendea kazi ambavyo vitaongeza ufasi wa utoaji huduma kwenye zahanati hizo
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.