Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Kata katika majimbo ya Chamwino na Mvumi, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino wameanza kupatiwa mafunzo ya siku 3 kuanzia leo tarehe 4 hadi 6 Agosti, 2025 kuhusu masuala mbalimbali ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani 2025.
Mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata, yamefunguliwa na mgeni rasmi Bi. Prudence Kaaya ambaye pia ni Msimamizi wa Uchaguzi wa majimbo ya Chamwino na Mvumi na yanafanyika ili kuwafanya kutekeleza majukumu yao ya kusimamia hatua mbalimbali za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Bi Kaaya amewapongeza washiriki kwa kuteuliwa na kuaminiwa kutekeleza na kusimamia shughuli za uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Halikadhalika, Ndg. Kaaya amewaaasa Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata kusoma katiba, sheria, kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo yote yanayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwani Tume hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia na kuratibu shughuli za Uchaguzi Mkuu wakati wa utekelezaji wa shughuli zao za Uchaguzi.
“Nachukua nafasi hii kuwaasa pamoja na uzoefu ambao baadhi yenu mpo nao katika kutekeleza shughuli za uchaguzi kusoma katiba, sheria, kanuni, taratibu na miongozo pia fuateni maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume katika kutekeleza shughuli za uchaguzi”. Alisema Bi. Kaaya
Pia amewahimiza kuzingatia kuvishirikisha vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili katika hatua zote kwa kuzingatia matakwa ya kikatiba, sheria, kanuni na maelekezo mbalimbali ya Tume, pamoja na kujiepusha kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.