Wananchi wa kijiji cha Chinangali II Kata ya Buigiri, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino leo Mei 6, 2025 wamepokea kwa furaha mradi wa ujenzi wa daraja na uchongwaji wa barabara ya Mabeo hadi Mpela yenye urefu wa kilomita 5.
Mradi huo umetambulishwa leo sambaba na kutambulishwa Mkandarasi Issa Amiri Kigaire katika Mkutano mkuu wa kijiji cha Chinangali II ambapo utahusisha ujenzi wa daraja kubwa la mawe lenye midomo 4 pamoja na uchongwaji wa kilomita 4 ya barabara ya kiwango cha changarawe ambapo jumla ya Shilingi milioni 261 kuakisi thamani ya mradi huo ambao utatekelezwa ndani ya kipindi cha miezi sita na kukamilika mwezi Oktoba, 2025.
Ujenzi wa daraja na barabara hiyo umekuja kufuatia kero ya muda mrefu ya Wananchi wa Chanangali II kuzunguka kwa umbali mrefu kufuata huduma za kijamii ikiwemo ya afya katika kituo cha afya Chamwino, hivyo mradi huo utasaidia kupunguza umbali na kuondoa kadhia hiyo kwa Wananchi pamoja na kuleta neema ya fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Chinangali II kwa kupata ajira mbalimbali kipindi cha utekelezwaji wa mradi huo.
Akizungumza wakati wa kutambulishwa mradi huo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri na Diwani wa Kata ya Buigiri Mhe. Kenneth Yindi ameelezea mradi huo utakavyoleta manufaa kwa Wananchi wa Chamwino kwa kuwa barabara hiyo kuwa katika mpango wa kuanza kutumika kama njia ya daladala kutoka Chamwino Ikulu hadi Dodoma Mjini ili kurahisisha usafiri.
Kwa upande wa Sargent. Imani John Mwakilama kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambapo barabara hiyo itapita katika eneo la Jeshi hilo amewaomba Wananchi hasa watakao bahatika kupata ajira wakati wa utekelezwaji wa mradi huo kuhakikisha hawafanyi vitendo vitakavyohujumu mradi huo.
Halikadhalika, Kaimu Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Chamwino amewahasa Wananchi kuhakikisha hawapitishi mifugo ikiwemo Ng’ombe ambao kwato zao huchangia kuharibu barabara ili barabara hiyo iweze kutumika kwa muda mrefu.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.