Shirika lisilo la kiserikali, Afya Plus limejenga vizimba vya kunawia mikono kwenye shule kadhaa za Halmashauri ya Chamwino, katika jitihada za kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakuwa na sehemu ya kunawa mikono kwa maji tiririka na hivyo kuepuka magonjwa yatokanayo na uchafu.
Hafla ya uzinduzi wa vizimba hivyo imefanyika leo Agosti 13, 2025 katika shule ya sekondari Chamwino na kuhudhuriwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Bi. Tulinagwe Ngonile (Afisa Elimu sekondari), baadhi ya Wakuu wa Idara za Halmashauri,wazazi, wanafunzi na walimu wa shule hiyo pamoja na viongozi mbalimbali kutoka shirika la Afya Plus.
Mwingine aliyeshiriki ni Afisa Afya Mkoa, Nelson Rumbeni ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa hafla hiyo, na mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Dodoma ambapo katika hotuba yake fupi amelishukuru shirika la Afya Plus kwa kujenga vizimba hivyo na kueleza kuwa vitakuwa chachu ya kuboresha afya za wanafunzi kwa kuwasaidia kujikinga na magonjwa yatokanayo na uchafu.
Vilevile amepongeza wadau wengine mbalimbali waliowezesha ujenzi wa vizimba hivyo wakiwemo wazazi ambao walitoa vifaa vya ujenzi vinavyopatikana katika maeneo yao kama vile mchanga na tofali.
Aidha, amewahimiza wanafunzi ambao ndio walengwa wa mradi huo kuwa walinzi ili uweze kudumu na kuendelea kuwahudumia.
Naye Mkurugenzi wa shirika la Afya Plus, Bi. Suzan Yumbe amebainisha kuwa Shirika lake litaendelea kutekeleza miradi mingine katika mkoa wa Dodoma ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyoo katika shule zenye uhitaji.
Shule zilizonufaika na mradi huo ni shule ya sekondari Chamwino, shule ya sekondari Buigiri, shule ya msingi Chamwino, Uguzi na Buigiri misheni.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.