Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino jana Februari 26, 2026 ikiwa na lengo la kuangalia maendeleo ya miradi hiyo.
Katika ziara hiyo Mhe. Senyamule aliongozana na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe, Janeth Mayanja, Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Tito Mganwa pamoja na wataalam mbalimbali kutoka ofisi yake na taasisi za Serikali zinazopatikana Wilaya Chamwino.
Miradi ya Maendeleo iliyotembelewa na kukaguliwa ni pamoja na ujenzi wa Zahanati ya Msanga, ujenzi wa daraja la mawe barabara ya Mpera, ujenzi wa shule ya Sekondari ya Amali-Nzali, ujenzi wa ofisi za Tanesco Wilaya ya Chamwino na shamba la zao la matufaa.
Akizungumza wakati akikagua mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Amali-Nzali Mhe. Senyamule amewaasa Wananchi hasa vijana wa Kijiji cha Nzali Kata ya Chilonwa kuchangamkia fursa za kiuchumi zitakazotokana na uwepo wa mradi huo mkubwa wa shule ya ufundi uliogharimu takribani shilingi za Tanzania bilioni 1.6.
"Kuwa na shule hii watoto wanakaa bweni hapa kwenu nyie ni fursa, hapa watakuwa wanahitaji kula mboga za majani, maharage, kula wali. Mkuu wa Shule akiwepo hapa awe anawaelekeza vijana waliopo karibu namna gani wapate tenda ili kuwepo kwa wale wageni kuwe kwao ni baraka". Alisema Mhe. Senyamule.
Sambamba na hilo, amewataka wananchi hao kuhakikisha wanatunza miundombinu ya shule hiyo moja katika Mkoa mzima wa Dodoma inayopatikana katika Kijiji cha Nzali kwani ni bahati kwao kupata mradi huo.
Aidha, amewataka pia Wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya uwepo wa mafua makali kwa kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono na kuosha mikono kwa maji tiririka ili kujikinga na maambukizi ya magonjwa hayo.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.