Baraza la wafanyakazi Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino leo Februari 27, 2026 limeketi kikao chake cha kikanuni kujadili na kupitisha mapendekezo ya mpango wa bajeti ya shilingi za Tanzania bilioni 57 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 pamoja na kufanya uchaguzi wa viongozi wapya wa kuliongoza baraza hilo.
Kikao hicho kilifunguliwa na mgeni rasmi na Katibu Tawala Wilaya ya Chamwino Ndg. Neema Nyalege na kuongozwa na Mwenyekiti wake Mkurugenzi Mtendaji, Ndg. Tito Mganwa. kilihudhuriwa pia na wajumbe kutoka vyama mbalimbali vya wafanyakazi, Menejimenti ya Halmashauri pamoja na wawakilishi kutoka kila idara na vitengo.
Akizungumzia moja ya mikakati iliyowekwa na Halmashauri ili kuongeza bajeti na mapato kwa mwaka wa fedha 2026-2027, Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa baraza hilo Ndg. Tito Mganwa amesema Halmashauri imetenga eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 6000 katika kijiji cha Chinangali II kinachopatikana katika barabara kuu ya kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya maegesho ya magari makubwa ya biashara.
Halikadhalika, wakati akiwasilisha bajeti hiyo Mchumi na Afisa Mipango wa Halmashauri Ndg. Elinlaa Kivaya ameeleza pia mikakati ya kuongeza mapato ikiwemo kuundwa kwa timu za ukusanyaji wa mapato na timu hizo kutoa mwenendo wa ukusanya wa mapato kila wiki kwa menejimenti ya Halmashauri pamoja na kuteuwa wasimamizi wa vyanzo vikubwa vya mapato na kupewa lengo la makusanyo kwa kila siku.
Mikakati mingine ni pamoja na kuendelea kutumia mfumo wa kieletroniki wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kwenye vyanzo vyote vya mapato pamoja na kuhimiza fedha zote zinazokusanywa kupitia mashine ya POS kuwekwa kwenye akaunti.
Aidha, Wajumbe pia walipata nafasi ya kupiga kura kuchagua viongozi wao wapya ambapo Ndg. Kuluthum Tangazo alishinda nafasi ya kuwa katibu wa baraza hilo na Ndg. Raymond Mwachango kuwa katibu msaidizi.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.